Header Ads Widget

Ticker

6/recent/ticker-posts

Obama aguswa na Hasheem Thabeet

Jina la mcheza kikapu nyota wa Ligi Kuu ya Mpira wa Kikapu Marekani (NBA), Mtanzania Hasheem Thabeet lilijitokeza jana katika hotuba fupi aliyoitoa Rais wa Marekani, Barack Obama wakati akizungumza na waandishi wa habari, ikulu jijini Dar es Salaam.

Obama ambaye alikuwa amefuatana na mwenyeji wake, Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete, alimtaja Thabeet kwa namna iliyoonyesha wazi kuwa anamfahamu vyema mchezaji huyo nyota wa timu ya Oklahoma City Thunder; huku akitania mwishoni mwa hotuba yake kwa kusema kuwa atamzungumzia siku nyingine.

Mtanzania Hasheem mwenye urefu wa mita 2.21, amejitwalia umaarufu mkubwa Marekani kutokana na uwezo wake uwanjani na pia kwa sababu hivi sasa ndiye mchezaji mrefu kuliko wote wanaocheza NBA.


Hasheeem alikwenda Marekani mwaka 2006 na kuanza kucheza NBA mwaka 2009 baada ya kusajiliwa na timu ya Memphis Grizzlies, hivyo kuandika rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kuwahi kucheza katika ligi hiyo yenye hadhi ya juu zaidi kwa mchezo wa mpira kikapu duniani.

Awali, kabla ya kuchomekea kwa utani jina la Hasheem katika hotuba yake, Obama alizungumzia namna Marekani inavyoshirikiana na Tanzania na mataifa mengine ya Afrika katika kukabiliana na changamoto mbalimbali kwa nia ya kusaidia harakati kuliendeleza bara hili.

ANENGUA 'LIVE' NGOMA YA MGANDA

Wakati akitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam akitokea Afrika Kusini, Obama alionekana kuvutiwa sana na ngoma mbalimbali za utamaduni alizochezewa wakati akipokelewa, zikiwamo za Mganda, Lizombe na Sindimba.

Kwa namna isiyotarajiwa, naye alijitosa na kuanza kunengua ngoma ya Mganda inayochezwa na wenyeji wa mkoa wa Ruvuma, huku akiungwa mkono na mwenyeji wake, Rais Kikwete na hivyo kuibua shangwe kubwa kutoka kwa wananchi waliokuwa wakishuhudia tukio hilo.

Kabla ya kuanza kucheza Mganda, Obama alianza kwa kumwaga tabasamu kuonyesha kuwa amevutiwa na ngoma hiyo, akawapigia makofi wachezaji na mwishowe akahitimisha hisia zake kwa kuanza kucheza.

Kabla ya Obama kutua, Rais Kikwete naye alionekana kuguswa na burudani ya ngoma zilizokuwapo uwanjani ambapo alikuwa akicheza kwa mtindo kama wa 'kiduku' muda mfupio kabla ya kuwasili kwa mgeni wake.

Katika hatua nyingine, mmoja wa watu waliofurahia salamu kwa kushikana mkono na kiongozi huyo alikuwa ni rais wa zamani wa klabu ya Yanga, Abbas Tarimba.

ZIARA YA OBAMA HAIMNUNUI RONALDO

Licha ya kuonekana kuwa ghali, gharama za jumla za ziara ya Rais Obama katika nchi tatu barani Afrika za Tanzania, Afrika Kusini na Senegal haikaribii hata kidogo fedha zilizotumiwa na klabu ya Real Madird ya Hispania kumnunua mshambuliaji wake Cristiano Ronaldo, imefahamika.

Kwa mujibu wa gazeti la Marekani la Washington Post, Obama na msafara wake watatumia dola za Marekani milioni 100 (Sh. bilioni 160) ili kujihakikishia usalama wakati wote wa ziara hiyo ambayo pia inawajumuisha mkewe Michele Obama na mabinti zake Malia na Sasha; kiasi ambacho ni kidogo kulinganisha na dau la paundi za England milioni 80 (Sh. bilioni 200) lililolipwa na Real Madrid kumtwaa Ronaldo kutoka Manchester United kabla ya kuanza kwa msimu wa 2009.

Hata hivyo, kiasi hicho cha fedha zinazotumiwa na Obama katika ziara yake Afrika (Sh. bilioni 160) kinalingana na bajeti za wizara tatu za serikali ya Tanzania kwa mujibu wa makadirio ya mapato na matumizi yaliyopitishwa bungeni mjini Dodoma hivi karibuni kwa mwaka wa fedha ulioanza jana wa 2013/2014.

Wizara ya Maliasili na Utalii imetengewa Sh. bilioni 75.6, Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Sh. bilioni 55.6 na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Sh. bilioni 30.3; hivyo jumla yao kuwa Sh. bilioni 161.5 ambazo ni sawa na gharama za ziara ya Obama barani.
 
Awali, baadhi ya Wamarekani walikuwa wakipinga ziara ya Obama barani Afrika kwa kudai kuwa ni ghali kwa taifa hilo, jambo ambalo limethibitika kuwa si sahihi na badala yake, ziara hiyo ina manufaa makubwa kiuchumi kwa Afrika na Marekani yenyewe kwani itasaidia pia kukuza fursa za kibiashara baina ya Afrika na taifa hilo.
 
CHANZO: NIPASHE

Yorum Gönder

0 Yorumlar